Saturday, 20 December 2014

ALI KIBA - MWANA






Ubora wa Msanii: Ni msanii mkongwe, mwenye jina, kipaji kikubwa mno na mashabiki lukuki

Kichupa kimetengezwa na: GodFather

Mahali kilipotengenezwa: Afrika Kusini

Maudhui ya wimbo: 

Wimbo wamuongelea namna "Mwana", binti aliyetokea mkoani katika familia yenye uwezo kifedha, anavyowatesa wazazi wake na anavyojitesa pia. Alipata kila kitu kwao lakini akatorokea Dar es Salaam kufuata ujana. Alifika jijini Dar es Salaam akiwa binti mzuri sana lakini akabadilika na kuwa "dakika mbili mbele nyuma" mpaka "kichwa kinauma" kwa kulewa, kutumia madawa na kila aina ya anasa za jiji! Ali anamalizia kwa kumsihi arudi nyumbani kwa wazazi wake kwa maana watafurahi sana akirejea. Ni kama hadithi ya mwana mpotevu katika biblia...

Dhima ya wimbo:

"Ujana ni giza na nuru". Kijana wapaswa kusikiliza ushauri wa watu wazima sababu huna busara kama wao - Ali anasema "Hujayajua mengi". Na usipowasikiliza utapotea katika lindi la uharibifu na kujutia - "mwenda tezi omo marejeo ngamani".

Mapokezi ya wimbo:

Baada ya kimya cha takribani miaka mitatu, Ali Kiba akaachia kibao hiki. Kila shabiki wa muziki alifurahia. Wimbo umesheheni mashairi yaliyoshiba na mdundo unachezeka kweli kweli. Wimbo ulipendwa na unapendwa kweli kweli. Si kumbi za starehe tu unakopigwa mara nyiingi sana, hata kwenye tamasha la Fiesta, alishangiliwa mnoooo alipoimba wimbo huu ambao kuna watu wengine wanasema ni fumbo-kejeli kwa msanii mwenzake mwenye jina kubwa Africa sasa hivi - Diamond.



Udadavuzi wa Kichupa:

Alama za Mzalishaji wa kichupa: 70%

Kama kawaida ya Bw. GodFather, kichupa hiki kina muonekano murua kabisa. Mwanga umechanganywa vizuri na rangi haziumizi macho. Kamera hairukiruki na shots za kichupa hicho zimechanganywa vema sana. Kama mzalishaji wa kichupa hiki, Bw. GodFather katutendea haki. Ila kama mzalishaji aliyebobea alitakiwa ajue maudhui ya wimbo anaouzalishia kichupa ili atoe ushauri yakinifu kuhusu namna ya kuzipanga scenes kuendana na maudhui ya wimbo. Hii ndio sababu, licha ya ubora va picha za video yenyewe, Bw.GodFather hajapata alama za juu sana.

Alama za Msanii kwenye kichupa: 30%

Kilichompeleka Ali kwa Madiba kutengeneza hiki kichupa ni nini? Kwani Adamu Juma asingeweza kufanya video ya ubora ule? kuna tofauti gani pale? Au ni ule ushamba wa kusikiliza maneno ya washika pembe mtaani wanaofikiri kwenda kwa Zuma tu ndio suluhisho la ubora wa video. Akajilazimisha kwenda wakati change hazitoshi? Maana zingetosha angebeba madancers wake au angelipia madancers wanaojua...sio wale maigizo tu!

Wimbo unahusu "Mwana wa Dar es Salama"...kuna Dar es Salaam kwa Madiba? Storyline hakuna.  Hatumuoni mwana.

Fashion mbaya kabisa! Ni msimu wa joto Afrika Kusini halafu Ali anavaa nguo za msimu wa baridi. Anapishana njiani na watu wamevaa T shirts na wengine wamekunja mikono mashati, yeye anajikunyata! Huu si ulimbukeni huu? Kwani hizo nguo si angenunua tu aje avae Arusha na Mbeya Juni mwakani?

Takribani dakika nzima inapotea kutuonesha anaangalia kioo, anavaa saa, miwani na headphones – kweli haya ni matendo tuliyoyategemea ya mtu aliyesema kiti chake kilikua na vumbi tu anapangusa halafu anakaa tena na kwamba Bw. Diamond Platnumz hajakalia kiti cha juu bali amekalia siti ya nyuma hukoooo... 


Shots za kwenye kiti hazina mantiki. Za nini na hafanyi kitu? Ukumbini kila mtu anaonekana kabisa anajua anachukuliwa video. Wapiga vyombo wanapapasa vyombo vyao badala ya kuvipiga... mzuka jukwaani upo wapiii?

Suala la madancers sio la kuficha. HAWAJUI KUCHEZA. Na wamecheza style mbili tu. Hakuna ubora wa upangaji wa madancers kucheza yani choereography. Ali angeiacha ile scene madancers wanafanya mazoezi akaongeza muda wa ukumbini na jukwaani ili kama kucheza kuonekane vizuri. Kwa nini asiende na madancers wake toka bongo? Au alichokichanga hakikutosha? Si yupo kwenye record label and management company ROCKSTAR4000 and Rockstar Publishing yule – sasa wale wameshindwa kusafirisha madancers wanaojua kucheza kibongo? Akaishia kucheza breakdance wimbo wa rhumba… Aibu tupu!!!

Ujumbe kwa Bw. Ali Kiba:

Bw. Ali,mtu akiboronga anapaswa kuambiwa ukweli. Hii video sio ya hadhi yako. Ni utumbo mtupu!!! Hivi kweli wewe uliyefikia levo ya kurekodi na R Kelly pamoja na mastaa wakubwaa Afrika kisha waenda kufanya kachupa kakishamba namna ile? Halafu wataka tukuite King of Bongo Fleva, seriously? Tutasifiaje shamba lililojaa michongoma?

Hii ingekuwa “behind the scene” video. Sio siri  ni mbaya kabisa. Kama busara ipo, waambie wenye vituo vya luninga ulikoipeleka wasiipige tena maana utapoteza mashabiki zaidi badala ya kuongeza. Mtafute mzalishaji wa vichupa hapa bongo akutengenezee kichupa kingine. NI HAYO TU!!!